Jeshi la Sudan laahidi kujibu shambulizi la wanamgambo wa RSF
Eric Buyanza
June 7, 2024
Share :
Jeshi la Sudan limesema litajibu vikali shambulizi la wanamgambo wa RSF katika kijiji cha Wad al-Noura siku ya Jumatano lililoua zaidi ya watu 100.
Shambulizi hilo lilikuwa ni kubwa zaidi katika msururu wa mashambulizi yaliyofanywa na RSF kwenye vijiji vidogo vidogo katika jimbo la Gezira linalosifika kwa kilimo.
Afisa wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan jana Alhamisi alitoa wito wa uchunguzi wa shambulizi hilo la Wad al-Noura.
"Licha ya hali mbaya katika mzozo wa Sudan, lakini picha zinazoonyeshwa kutoka kwenye eneo hilo zinaumiza sana," alisema Mratibu huyo wa Masuala ya Kiutu Clementine Nkweta-Salami kwenye taarifa yake.
Wanamgambo wa RSF sio tu waliwashambulia wanakijiji, bali pia kupora mali zao na kuwafanya wanawake na watoto kukimbilia kwenye mji jirani wa Managi kuomba hifadhi.
Wanamgambo hao walianzisha mapigano na jeshi la Sudan mwezi Aprili, 2023 kufuatia mzozo baina ya majenerali wawili wa jeshi na tangu hapo wamechukua udhibiti wa mji mkuu Khartoum na maeneo mengi ya magharibi mwa Sudan.