Jeshi laruhusu ndevu baada ya marufuku ya miaka 100
Eric Buyanza
March 29, 2024
Share :
Wanajeshi wa Uingereza sasa wataruhusiwa kufuga ndevu baada ya Jeshi la nchi hiyo kubatilisha marufuku ya miaka 100, gazeti la Telegraph linaripoti.
Mfalme, ambaye ndiye Amiri Jeshi Mkuu, alitia saini uamuzi huo siku ya jana (Alhamisi) kuwaruhusu maafisa na askari wote kuanza kufuga ndevu.
Sera hiyo mpya itaanza kutumika leo (Ijumaa) ili wanajeshi walio likizo ya Pasaka wawe na maandalizi mazuri ya kuandaa videvu vyao.
Mkuu wa Jeshi Jenerali Sir Patrick Sanders, anasema baada ya mapitio ya sera ya Jeshi kuhusu ndevu, wengi waliona Jeshi linahitaji kubadilisha sera hiyo na kuruhusu askari wake kufuga ndevu.
Hili limekuja baada ya Grant Shapps, Katibu wa Ulinzi, kusema marufuku ya ndevu yalikuwa ni ya 'Kijinga'.
Hata hivyo, wanajeshi wamepewa masharti ya kwamba ndevu hizo lazima ziwe "nadhifu" zimepambwa vizuri na zitakaguliwa mara kwa mara.