João Pedro ananikumbusha Karim Benzema - Xabi Alonso
Eric Buyanza
September 12, 2026
Share :

Kocha wa Chelsea, Xabi Alonso, amemwagia sifa lukuki mshambuliaji wake João Pedro, akieleza kuwa mchezaji huyo ana sifa nyingi zinazomfanya amkumbuke mshambuliaji wa zamani wa Real Madrid, Karim Benzema.
Sifa hizo kutoka kwa kocha huyo raia wa Uhispania zimekuja mara baada ya João Pedro kutangazwa rasmi kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi Agosti wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), kufuatia mwanzo mzuri wa msimu ambapo amekuwa nguzo muhimu kwenye safu ya ushambuliaji ya klabu hiyo ya London Magharibi.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari kuelekea mechi yao inayofuata dhidi ya Hull City, Alonso alieleza kuwa uwezo wa João Pedro wa kucheza maeneo tofauti uwanjani unamfanya kuwa mshambuliaji wa kipekee sana.
"Katika mambo mengi ananikumbusha Benzema," Alonso aliiambia BBC Sport.
"Ni kwa sababu ni mzuri akiwa ndani ya boksi, ni mzuri nje ya boksi, anajua kukata akitokea upande wake wa kushoto, na ni mzuri wa vichwa. Ni mchezaji aliyekamilika na mwenye akili kubwa ya mpira."
Alonso, ambaye aliwahi kucheza na Benzema wakiwa Real Madrid, aliongeza kuwa wasifu wa João Pedro unamuwezesha kufanya kila kitu uwanjani, kuanzia kushuka chini kuchezesha timu hadi kukaba na kufunga.
Nyota huyo wa Brazil alimaliza msimu uliopita akiwa na mabao 20 katika mechi 50, na sasa amebeba jukumu kubwa la kuongoza mashambulizi ya Chelsea.





