Julian Alvarez aripotiwa kukabaliana na changamoto ya Afya ya Akili.
Joyce Shedrack
August 28, 2026
Share :
Mshambuliaji wa Atlético Madrid, Julián Álvarez, anadaiwa kukabiliwa na changamoto za afya ya akili hali ambayo imemfanya akose baadhi ya vipindi vya mazoezi ya timu hiyo huku sababu za wazi siku moja iliyopita zikitajwa ni maumivu ya tumbo jambo ambalo kwa sasa linaripotiwa tofauti.

Taarifa kutoka Hispania zinaripoti kuwa hali hiyo imemfanya Alvarez akose mazoezi ya timu tangu Jumatano katika kituo cha mazoezi cha Majadahonda huku taarifa rasmi za klabu zikieleza tofauti kuwa nyota huyo amekosa mazoezi kutokana na kuwa na usiku mbaya na maumivu ya tumbo.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26 alikumbana na mazingira magumu kutoka kwa baadhi ya mashabiki wa Atlético baada ya kuingia uwanjani alizomewa na kushangiliwa kwa kejeli kutokana na taarifa kwamba anatamani kujiunga na Barcelona.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Álvarez anahitaji muda pamoja na msaada unaofaa katika kipindi hiki kigumu, huku afya na ustawi wake vikiwa jambo la muhimu zaidi.
Wakati huo huo, taarifa zinaeleza kuwa kuchezea Barcelona bado ni moja ya ndoto binafsi za mshambuliaji huyo wa Argentina licha ya klabu yake kusisitiza siku ya jana kuwa hawatamuuza kwenda Barcelona kamwe.





