Kabila na Nangaa wakutana na Uwakilishi wa UN
Sisti Herman
November 4, 2026
Share :

Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC (MONUSCO), James Swan amekutana mjini Goma na viongozi wa muungano mpya wa kisiasa na kijeshi wa FRN unaoongozwa na Rais wa zamani Joseph Kabila.
Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais wa FRN, Bertrand Bisimwa amesisitiza kuwa kundi hilo bado lina nia ya kuendelea na mchakato wa amani wa Doha.
Hata hivyo, Bisimwa ameonya kuwa mpango wa Rais Félix Tshisekedi wa kubadilisha katiba ya nchi utavuruga kabisa makubaliano yote ya amani yaliyofikiwa.
Wakati huo huo, muungano huo wa FRN umepinga vikali mpango wa kurefushwa kwa muda wa kuhudumu wa MONUSCO ukidai kuwa ujumbe huo umefeli katika miaka yake 28 ya uwepo nchini humo na unapaswa kuondoka kikamilifu.
Kwa upande wake, MONUSCO imetoa ujumbe mzito ikisisitiza umuhimu wa kuheshimu michakato ya amani na usitishwaji wa mapigano mashariki mwa nchi hiyo.
James Swan amesisitiza kuwa mawasiliano yao na vikundi vyenye silaha yanalenga kulinda raia, kufuatilia usitishwaji wa mapigano na kuruhusu mashirika ya kibinadamu kuwafikia wananchi wanaoteseka.
MONUSCO imebainisha kuwa mkutano huo ni mwendelezo wa juhudi za utekelezaji wa majukumu yake ya kiusalama.





