Karibu 20% ya dawa za kansa Afrika ni duni au feki
Eric Buyanza
July 2, 2025
Share :
Barani Afrika, dawa za saratani zimegundulika kuwa duni au bandia, hali inayomaanisha kuwa wagonjwa wamekuwa wakipewa dawa ambazo ama hazifanyi kazi au zinaweza hata kuwadhuru.
Takwimu mpya zinaonyesha kuwa idadi kubwa ya watu huenda wanatumia dawa ambazo hazina viambato muhimu vinavyohitajika kuzuia au kupunguza kasi ya saratani. Hayo ni kulingana na utafiti uliochapishwa wiki hii na jarida la The Lancet Global Health, uliochunguza sampuli kutoka hospitali 12 na maduka ya dawa 25 katika nchi za Ethiopia, Kenya, Malawi na Cameroon.
Watafiti walijaribu karibu aina 200 za dawa za saratani kutoka kampuni tofauti. Matokeo yalionyesha kuwa karibu asilimia 17 ya dawa hizo, sawa na moja kati ya dawa sita, zilikuwa na viwango visivyo sahihi vya viambato hai, hata zile zilizotumika katika hospitali kubwa.
Dawa zenye viambato visivyotosha zinaweza kushindwa kudhibiti uvimbe wa saratani, na hata kusababisha usambaaji wake zaidi mwilini. Ingawa visa vya dawa duni za antibiotiki, malaria na kifua kikuu vimeripotiwa awali, huu ndio utafiti wa kwanza kufichua kiwango kikubwa cha dawa bandia za saratani barani Afrika.
Lutz Heide, mtaalamu wa famasia kutoka Chuo Kikuu cha Tübingen nchini Ujerumani, alisema hakushangazwa na matokeo hayo. Ingawa hakuhusika moja kwa moja katika utafiti huo, alisifu ripoti hiyo kwa kutoa mwanga juu ya suala hilo.
Sababu za tatizo hili ni nyingi na si rahisi kuzikabili moja kwa moja. Kwa mujibu wa Marya Lieberman wa Chuo Kikuu cha Notre Dame nchini Marekani, alieongoza utafiti huo - sababu zinaweza kuwa kasoro katika utengenezaji, hali mbaya za hifadhi, au uwepo wa bidhaa bandia kabisa. Dawa bandia huongeza uwezekano wa tofauti kubwa kati ya kilicho kwenye lebo na dawa halisi.
Kutambua dawa duni au bandia ni changamoto kubwa. Mara nyingi, wataalamu wa afya au wagonjwa hulazimika kutegemea uchunguzi wa macho — kama vile kuangalia rangi au maandiko ya dawa. Lakini katika utafiti huu, ni chini ya robo moja ya dawa duni zilizogundulika kwa njia hiyo. Zilizosalia zilibainika kupitia uchunguzi wa maabara.
DW