Katiba imara ni muhimu kwa Maendeleo
Sisti Herman
August 21, 2024
Share :
Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa ACT Wazalendo, Abdul Nondo amesisitiza umuhimu wa kuwa na Katiba imara na yenye nguvu kama sehemu ya kuchochea maendeleo ya Tanzania na kukuza ufanisi wa kitaasisi.
Nondo ni miongoni mwa Wanasiasa kutoka Baraza la Vyama vya Siasa Nchini ambaye leo Jumatano August 21, amejumuika na Wanasiasa wengine Jijini Dar es salaam kutoa maoni yao kuhusu uandishi wa dira mpya ya maendeleo ya mwaka 2050 katika mkutano ulioandaliwa na Ofisi ya Rais Tume ya Mipango.
“Katiba ndio msingi mkubwa kabisa utakaokuja kuleta maendeleo haya tunayoyazungumza, Katiba italeta utaasisi, italeta utawala wa sheria, tumeona tumepata Viongozi ambao wanafanya maamuzi ya hovyo hata kiasi cha kukimbiza Wawekezaji, tuweke misingi imara ambayo itatuletea uchumi imara n.k”
Katika hatua nyingine, Nondo ameshauri kuwa kuelekea mwaka 2050 ni muhimu Serikali iongeze kasi katika urasimishaji wa shughuli zisizo rasmi kwa kuwawezesha mitaji na kutengeneza mazingira mazuri kwa ajira ambazo bado hazijaingia kwenye mifumo iliyo rasmi.