pmbet

Kenya na Tanzania kwenye sakata la ndege!

Eric Buyanza

January 16, 2024
Share :

Kenya na Tanzania zimesema zinafanya juhudi kuutatua mvutano uliozuka baina ya nchi hizo mbili baada ya Tanzania kutangaza kufuta kibali cha safari za ndege za shirika la Kenya Airways kati ya Nairobi na Dar es Salaam.
 

Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini Tanzania, TCAA,  ilitangaza mnamo Jumatatu jioni kufuta kibali hicho kwa ndege za shirika hilo la Kenya kujibu msimamo wa serikali mjini Nairobi wa kukataa kutoa kibali cha kuingia Kenya kwa ndege za mizigo za kampuni ya ndege ya Tanzania.

Tangazo la TCAA lilisema ndege zote za Kenya Airways kutokea Nairobi hazitaruhusiwa kutua mjini Dar es Salaam kuanzia Januari 22.
 

Hata hivyo Mawaziri wa Mambo ya Kigeni wa nchi hizo mbili, wamesema wamefanya mawasiliano kwa njia ya simu na kukubaliana kuutafutia ufumbuzi mvutano uliojitokeza katika kipindi cha siku tatu zinazokuja.
 

Mawaziri hao January Makamba wa Tanzania na mwenzake wa Kenya, Musalia Mudavadi, wamethibitisha taarifa hizo kupitia ujumbe katika kurasa zao za mtandao wa kijamii wa X zamani ukijulikana kama Twitter.
 

Makamba amesema wamekubaliana na Mudavadi kwamba "vizuizi vya usafiri wa anga kati ya nchi zetu" na kutoka miongoni mwa nchi hizo kwenda nchi nyingine haupaswi kuwepo.
 

TCAA YASEMA UAMUZI WAKE DHIDI YA KENYA ULIKUWA NI WA ´KUJIBU MAPIGO´

Katika taarifa ya awali ya TCAA, mamlaka hiyo ilisema uamuzi wa kuzuia ndege za Kenya Airways ulikuwa ni ´kujibu mapigo´ kwa msimamo wa Kenya kuzuia ndege za mizigo za Air Tanzania.
 

TCAA imesema Kenya iliinyima Air Tanzania kibali kwa ndege zake za mizigo kufanya safari baina ya nchi hizo mbili na kutoka Kenya kwenda nchi nyingine.
 

Kulingana na mamlaka hiyo, msimamo huo wa Kenya ni kinyume na makubaliano kati ya nchi hizo mbili kuhusu sekta ya usafiri wa anga yaliyotiwa saini mwaka 2016.

pmbet
pmbet

Leagues standings

Tanzania Premier League
pmbet
pmbet