KETE MPYA YA MARESCA: Amfuata Koné kurudisha heshima ya Man City
Eric Buyanza
August 20, 2026
Share :

Wakati tukielekea mwishoni mwishoni kabla ya kufungwa kwa dirisha kubwa la usajii, Klabu ya Manchester City imeingia rasmi kwenye mbio za kutaka kumsajili kiungo wa AS Roma na timu ya taifa ya Ufaransa, Manu Koné.
Man City wamemgeukia Koné mwenye umri wa miaka 25 baada ya kumuuza kiungo Tijjani Reijnders kwenda klabu ya Al-Qadsiah ya Saudi Arabia.
Kikosi hicho chini ya kocha Enzo Maresca kinahitaji kiungo mwenye nguvu, kasi, na uwezo mkubwa wa kuzuia na kushambulia ili kuongeza uhai katikati ya uwanja.
AS Roma wanahitaji kiasi cha pauni milioni 51 (sawa na Shilingi za Tanzania Bilioni 182) ili kumuachia kiungo huyo. Thamani yake ilipanda baada ya kuonyesha kiwango kikubwa kwenye Kombe la Dunia.
Manchester United walikuwa wa kwanza kufanya mazungumzo na wawakilishi wa mchezaji huyo, hata hivyo walirudi nyuma kutokana na bei kuwa kubwa, jambo lililotoa mwanya kwa Manchester City kujichomeka.





