Kigoda kinachokaliwa na wanaume pekee, wanawake ni marufuku
Eric Buyanza
July 8, 2026
Share :

Vigoda vina nafasi muhimu kwenye maisha ya kila siku ya jamii za kiafrika, Wamasai, ni miongoni mwa jamii ya kiafrika zinazotumia kigoda, ingawa kwao ni mahsusi tu kwa ajili ya wanaume, kwa sababu ni marufuku kwa mwanamke kukikalia.
Kiasili, wanaume hutumia vigoda kutangaza kuwa yuko njiani na kuelekea nyumbani kwa mkewe. Aghalabu wamasai wana utamaduni wa kuoa mke zaidi ya mmoja na wote wanaishi kwenye mji mmoja.
Hata hivyo, kila mke ana kijumba chake ambako mume wao wa pamoja humtembelea kwa kufuata ratiba yake ya siri. Nyumba ya mzee wa mji hujengwa katikati, na kigoda hicho maalum ambacho hutengenezwa kwa kutumia mti maalum, hutumiwa kutangaza uwepo wake rasmi na pia ni ishara ya mamlaka na adhama.
Kabla ya kuwasili bomani, mshenga anatumwa kupeleka kigoda hicho kwa mke atakayempokea. Pindi mke anapokiona na kukabidhiwa kigoda kile, ujumbe wa kuwa mumewe yuko njiani umemfikia. Maison loldapash, mkaazi wa tiamamut kaunti ya laikipia nchini Kenya, anafafanua umuhimu wa kigoda hicho kwa wamasai na anasisitiza kuwa mwanamke anapokikalia, hufikwa na mkosi.
''tumeishi tukijua hiki kigoda sio cha kuchezewa. Nimewahi kushuhudia mama mmoja ambaye nilimpeleka hospitali kule kimanjo. Alichukua kile kigoda na kuingia nacho bafuni. Alipoinuka tu kujipaka sabuni, mama huyo alianguka na akaumia vibaya sana,'' alisema loldapash.
Kulingana na loldapash, mwanamke huyo aliyekuwa na ujauzito wa miezi sita, alitokwa damu nyingi sana na alimkimbiza hospitali. Anasema kwa bahati mbaya mwanamke huyo alifariki dunia. Anabainisha kuwa jambo hilo ni sawa na laana.
Kimsingi, kigoda hicho kinaashiria unyumba na wajibu wa mwanaume katika jamii wa kuiongoza familia.
Ujumbe maalum wa kigoda hicho ni kuikumbusha jamii kuhusu wajibu wa mwanaume na majukumu yake katika jamii za kiafrika.
DW





