Kijana aliyempeleka kuku wake mgonjwa hospitali awa gumzo
Eric Buyanza
June 19, 2026
Share :

Kijana Markos Abaaye mwenye umri wa miaka 12 kutoka nchini Ethiopia amekuwa gumzo katika mitandao ya kijamii baada ya kuchukua hatua isiyo ya kawaida ya kumpeleka kuku wake mgonjwa katika hospitali inayotibu binadamu ili apatiwe matibabu.
Kuku huyo aliyepewa na wazazi wake, kwa Markos alikuwa wa thamani kubwa kwake, kiasi kwamba alimchukulia kama sehemu ya familia.
Baada ya kuku wake kuanza kuugua na hali kuzidi kuwa mbaya akiwa hana suluhisho jingine, aliamua kumpeleka hospitali.
"Nilidhani hospitali ni mahali ambapo viumbe wote wagonjwa wanaweza kutibiwa," Markos alinukuliwa akisema.
Tukio hilo lilitokea katika Hospitali ya Denbecha, ambako muuguzi Omar Chan alimwona kijana huyo akiwa amembeba kuku wake kwa huzuni kubwa usoni.
Kwa mujibu wa muuguzi huyo, watu wengi waliokuwepo hospitalini walishangazwa na kitendo hicho, huku baadhi wakijaribu kumcheka. Lakini yeye aliona jambo tofauti.
"Niliona huruma kubwa kwenye uso wa mtoto huyo. Alikuwa na wasiwasi wa kweli kuhusu afya ya kuku wake. Hakukuwa na mzaha katika alichokuwa akifanya," alisema.
Baada ya kufafanuliwa kuwa hospitali hiyo hutibu binadamu pekee, Markos alielekezwa kwenda kwa wataalamu wa mifugo.
Maelfu ya watu waliguswa na upendo na huruma aliyoonyesha kwa mnyama wake. Ndani ya muda mfupi, simulizi yake ikawa maarufu nchini Ethiopia na nje ya mipaka yake.
Umaarufu wa Markos uligeuka kuwa baraka baada ya makampuni na watu kadhaa kumzawadia zawadi mbalimbali, ikiwemo kuku ambapo kampuni ya Trust Agro ilimzawadia vifaranga vya kuku 100 kutokana na moyo wake wa kujali wanyama.
Mbali na zawadi hiyo, taasisi hiyo iliahidi kugharamia malazi, chakula na mafunzo maalumu ya ufugaji wa kuku kwa kijana huyo.
BBC





