Kim Jong Un apanga kurusha satelaiti tatu za kijasusi
Eric Buyanza
January 1, 2024
Share :
Korea Kaskazini inapanga kurusha satelaiti nyingine tatu za kijasusi mwaka ujao kama sehemu ya juhudi za kuimarisha jeshi lake, vyombo vya habari vya serikali ya nchi hiyo vimesema.
Mwezi uliopita Pyongyang iliweka satelaiti ya kijasusi angani na inadai kuwa tangu wakati huo imepiga picha maeneo makubwa ya kijeshi ya Marekani na Korea Kusini.
Akielezea malengo yake ya 2024, Kim Jong Un pia alisema kuwa shughuli zake na Korea Kusini zitapata "mabadiliko ya kimsingi".
Na alisema hakuwa na namna ila kusonga mbele na matarajio yake ya nyuklia.
Akizungumza katika mkutano wa mwisho wa mwaka wa Chama tawala cha Wafanyakazi cha Korea, Bw Kim alisema kuungana na Korea Kusini sasa haiwezekani tena.
Alisema Seoul inachukulia nchi yake kama adui. Inaonekana kuwa ni mara ya kwanza kwa Bw Kim kusema jambo kama hilo na kuashiria mabadiliko rasmi katika sera, ingawa kiutendaji kumekuwa na matarajio madogo ya kuungana kwa miaka kadhaa, bila mafanikio na juhudi kidogo kufanywa.
Uhusiano kati ya nchi hizo mbili uko katika hali mbaya.
Mwezi uliopita, baada ya kurushwa kwa satelaiti ya kijasusi, Pyongyang ilivunja makubaliano na Seoul ambayo yalilenga kupunguza mvutano wa kijeshi.
Korea Kaskazini pia iliendelea na majaribio ya mara kwa mara ya makombora yake mwaka mzima wa 2023 na mapema mwezi huu ilirusha kombora lake la juu zaidi la masafa marefu, na kukaidi vikwazo vya Umoja wa Mataifa.
Kurushwa kwa kombora la balestiki linalovuka mabara, ambalo lina masafa ya kufika katika bara la Amerika Kaskazini, kulizua shutuma za mara moja kutoka Magharibi.
Wakati huo huo Korea Kaskazini haijafurahishwa na Korea Kusini kuimarisha ushirikiano wa kiulinzi na Marekani, baada ya manowari ya Marekani yenye silaha za nyuklia kufika katika maji yake.