Kisa Barbara, mashabiki wamjia juu Harmonize afuta Post
Joyce Shedrack
April 23, 2024
Share :
Msanii wa bongofleva nchini Harmonize ameonesha kuchukizwa na maoni ya mashabiki kwenye chapisho lake alilochapisha kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii Instagram inayomhusisha aliyekuwa Afisa Mtendaji Mkuu wa (C.E.O) wa klabu ya Simba Barbara Gonzalez baada ya kufuta chapisho hilo.
Siku ya jana Harmonize alichapisha picha ya Barbara nakuandika maneno yafuatayo;
"Tatizo lilianzia hapa!!! Nazikumbuka nyakati za Simba ya C.E.O Barbara NDUGU ZANGU watani mnayo nafasi ya Kujiuliza!!! Ni suala la kuheshimu mwanamke tu na kumpa heshima!!! Siamini kama Barbara hana Mapenzi na SIMBA TENA!!! Kwa sababu nakumbuka jinsi alivyoipigania timu yenu !!! Mtaje Mohammed Dewji (Mwekezaji wa Simba) MARA NYINGI Uwezavyo aone nguvu ya MWANAMKE HUYU Kama unaipenda timu yako na unaamini Tatizo ni Usajili Tuu ila SIMBA SIO MBOVU na bado Unaipenda timu SIMBA".
Huo ulikuwa ni ujumbe wa Harmonize kwa C.E.O huyo wa zamani wa klabu ya Simba ambaye alionyesha kufurahishwa na ujumbe huo baada ya kuweka maoni yake kwa kuandika "Asante Kaka".
Ikumbukwe Harmonize ni shabiki wa klabu ya Yanga na ameonekana kutofurahishwa na kinachoendelea hivi karibuni kwa upande wa watani wao wa jadi Simba ambao wamekuwa na mfululizo mbaya wa matokeo ndani ya uwanja.
Baada ya chapisho hilo mashabiki wa Konde walionekana kumshambulia kwenye comments huku wengine wakimtaka aachane na masuala ya mpira jambo ambalo linahisiwa pengine ndo chanzo cha Harmonize kufuta ujumbe huo.