Kisa kuikimbia Simba Queens, JKT wakatwa alama ligi ya wanawake
Sisti Herman
February 4, 2024
Share :
Kamati ya soka la wanawake iliyo chini ya shirikisho la soka nchini (TFF) kupitia kifungu cha 32; 1-3 cha kanuni za ligi kuu ya wanawake 2023, imeamua kuipoka JKT Queens alama 5 na faini Tshs 3,000,000/= baada ya kugomea mchezo dhidi ya Simba Queens uliokuwa ufanyike tarehe 9 January 2024 kwenye uwanja wa Chamazi.
Kamati pia imewazawaidia Simba Queens alama 3 na mabao 3 kwa mujibu kanuni ya 18:45 ya ligi kuu ya wanawake 2023.
Kamati hiyo ya soka la wanawake pia imemfungia Katibu Mkuu wa JKT Queens Duncan Malyabana kutojishughulisha na shughuli za mpira wa miguu kwa kipindi cha miezi 12 kwa kuzingatia kifungu cha 32:1-5 cha kanuni za ligi kuu ya wanawake 2023 huku pia ikimshitaki kwenye Kamati ya maadili ya TFF Afisa habari wa timu hiyo Masau Bwire kwa kile kilichoitwa kusema taarifa za uongo kuhusu mchezo huo na kuzua taharuki kubwa.
JKT Queens hawakutokea uwanjani kucheza mchezo huo uwanja wa Chamazi wakitaka kutumia uwanja wao wa Major General Isamuyo ulioko Mbweni jijini Dar es Salaam hali iliyoleta mvutano na TFF ambao walipanga mchezo uchezwe Chamazi.