Kisa mwanae aliyefariki Davido afuta kesi mahakamani.
Joyce Shedrack
July 6, 2024
Share :
Nyota wa muziki Nchini Nigeria Davido ameifuta kesi aliyokuwa amemfungulia mpenzi wake wa zamani na mzazi mwenzake Sophia Momodu juu ya malezi ya binti yake wa kwanza anayeitwa Imade Adeleke baada ya Sophia kumuhusisha kwenye kesi hiyo aliyekuwa mtoto wa Davido na Chioma marehemu Ifeanyi aliyefariki mwaka 2022.
Wiki chache zilizopita Davido alimfungulia kesi Sophia ambaye ni mama wa binti yake ya juu ya malezi ya binti yao na kuiomba mahakama impe haki ya kumlea mtoto wake yeye mwenyewe .
Hivi karibuni kumekuwa na nyaraka za mahakamani zinazosambaa kwenye mitandao zikionyesha hoja za mwadada huyo kupinga ombi la Davido kukabidhiwa haki ya malezi ya mtoto wao akidai kuwa hakubaliani na msanii huyo kupewa malezi ya mtoto wao aitwaye ‘Imade’ kwani Davido hana malezi mazuri.
Kupitia nyaraka hizo Sophia alikitumia kifo cha mtoto wa Davido na Chioma ‘Ifeanyi’ aliyefariki kwa kuzama kwenye Bwawa la kuogelea nyumbani kwao kama ushahidi na kueleza kuwa malezi ya staa huyo ni hatari kwa mtoto wao.
Mwanadada huyo aliongezea kwa kudai kuwa kwa sasa Davido ameoa mwanamke mwingine hivyo malezi ya mtoto wao hayatokuwa salama huku akiiomba mahakama isitoe idhini ya Davido kumlea mtoto huyo na kusisitiza kuwa kutokana na kazi ya Sanaa ya msanii huyo amekuwa mtu wa kusafiri na nyumbani kwake kumekuwa na marafiki wengi wakiume hivyo kitendo hicho siyo salama kwa mtoto wao wa kike.
Kupitia ukurasa wake wa X Davido ameandika ujumbe unaonyesha kuumizwa na hoja za mwadada huyo hasa kumuhusisha marehemu mwanae kwenye kesi hiyo .
“Unaleta mada ya kifo cha mtoto wangu kila likija swala la madai ya malezi ya mwanangu huku ukijua swala hilo linatuumiza mimi na mke wangu kila siku kwenye maisha yetu, Imade atakuwa mkubwa na ataona jinsi nilivyompambania kwa sasa wewe kuwa nae kwani mwanangu hawezi kuwa mtoto kila siku atakuwa tu” ameandika Davido.