Kizimbani kwa kutaka kumuhonga Afisa wa TAKUKURU milioni 3
Eric Buyanza
February 6, 2024
Share :
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Morogoro, imemkamata na kumfikisha mahakamani Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa shule, Suleiman Mwishehe kwa tuhuma za kujaribu kumhonga Afisa wa TAKUKURU kwa kutoa shilingi 3,000,000 ili asifikishwe mahakamani wakati wa uchunguzi kwa ubadhilifu wa shilingi milioni 90 za ujenzi kwenye Kijiji cha Mlilingwa wilayani Morogoro.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Morogoro, Manyama Tungaraza alisema mshtakiwa huyo alikiri kosa na kutiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela au kulipa faini ya shilingi laki tano ambapo alilipa faini huku fedha alizotoa kama hongo kutaifishwa na kuwa mali ya Serikali.
Hata hivyo alisema mtuhumiwa huyo amefunguliwa jarada lingine mahakamani la kesi ya ubadhilifu wa Milioni 90 zilizoidhinishwa na kungizwa kwenye akaunti yake kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya walimu na chumba cha darasa, ujenzi ambao ulitakiwa kuwa umeshakamilika huku ukiwa bado haujakamilika.