"Klopp akiondoka sijui kama ntabaki" - Van Dijk
Joyce Shedrack
January 30, 2024
Share :
Nahodha wa klabu ya Liverpool, Mholanzi Virgil van Dijk amesema hana uhakika kama atakuwa sehemu ya timu hiyo baada ya kocha Jurgen Klopp kuondoka, Jurgen Klopp alishangaza wengi baada ya kutangaza kuondoka Liverpool mwishoni mwa msimu huu.
Alipoulizwa kama atakuwepo katika enzi nyingine mpya, Van Dijk amesema: “Swali gumu. Sijui.”
“Klabu itakuwa na kazi kubwa, hilo linafahamika, Kuziba nafasi sio tu ya meneja bali wafanyakazi [waandamizi] wote, mambo mengi yatabadilika. Nina kiu ya kufahamu mwelekeo gani utachukuliwa, lakini hilo litatangazwa na tutaona hali zetu.”amesema Van Dijk, mara baada ya mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Norwich ambapo walishinda 5-2.
Van Dijk alisajiliwa na Klopp kutoka Southampton kwa Pauni milioni 75, Januari 2018. Mkataba wa beki huyo unamalizika mwaka 2025.
Tangu ajiunge na Liverpool Van Dijk ameshinda mataji saba, Kombe la Dunia ngazi ya klabu (2019),UEFA Super Cup (2019), Champions League (2019),Premier League 2019/20, Carabao Cup 2022, FA Cup 2022, FA Community Shield 2022.
Liverpool mpaka sasa wanawania makombe manne, ikiwa ni Kombe la FA, wanaongoza Ligi Kuu ya Uingereza , wameingia fainali ya Kombe la Carabao, na wameingia 16 bora ya Ligi ya Europa.
Mameneja wasaidizi Pepjin Lijners, Peter Krawietz, na kocha wa kukuza vipaji Mitor Matos, pia wataondoka Liverpool, pamoja na Klopp.