Kocha wa Azam apata ulaji timu ya Taifa Libya
Sisti Herman
April 18, 2025
Share :
Aliyekuwa kocha mkuu wa Azam FC, Youssouph Dabo amesema ni heshima kubwa kupata nafasi ya kuifundisha timu ya taifa ya Libya, akiwa kocha msaidizi wa Aliou Cisse, aliyeipa Senegal ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), mwaka 2022.
Dabo alijiunga na AS Vita Club baada ya kuachana na Azam, Septemba 3, 2024, kutokana na mwenendo mbaya wa matokeo ndani ya timu hiyo uliopelekea kutolewa mapema katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa msimu wa 2024-2025.
“Kwa sasa nipo Ufaransa lakini nikiri wazi nimepata nafasi ya kujiunga na timu ya taifa ya Libya nikiwa kocha msaidizi, suala la kuondoka kwangu AS Vita Club na sababu siwezi kuliweka wazi ila mashabiki wangu watambue hilo,” alisema Dabo.
Raia huyo wa Senegal alisema hakuna tofauti kubwa ya kufundisha timu ya taifa au klabu isipokuwa majukumu ni yaleyale, hivyo ameamua kutafuta changamoto mpya na jambo kubwa ni fursa ya kufanya kazi pamoja na kocha mzoefu, Aliou Cisse.
Dabo aliondoka Azam FC Septemba 3, 2024, baada ya kuiongoza katika mchezo mmoja wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2024-2025, dhidi ya JKT Tanzania uliopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Mbweni na kuisha kwa suluhu, Agosti 28, 2024.
Kwa msimu wa 2024-2025, Dabo aliiongoza Azam katika michezo mitano, akianza na nusu fainali ya Ngao ya Jamii kwa ushindi wa mabao 5-2, dhidi ya Coastal Union, Agosti 8, 2024, kisha kuchapwa fainali na Yanga kwa mabao 4-1, Agosti 11, 2024.
Baada ya hapo, akaiongoza katika michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali ambapo alitolewa kwa jumla ya mabao 2-1, dhidi ya APR ya Rwanda, kufuatia kushinda nyumbani bao 1-0, Agosti 18, 2024, kisha kuchapwa ugenini 2-0, Agosti 24, 2024.
Dabo alijiunga rasmi na Azam FC Mei 1, 2023, baada ya kuachana na Klabu ya ASC Jaraaf de Dakar ya kwao Senegal ambako alitua kwenye timu hiyo kwa mkataba wa miaka mitatu akichukua nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa kocha, Kally Ongala.