Kocha wa Ufaransa aihofia Senegal na Norway Kombe la Dunia.
Joyce Shedrack
December 6, 2025
Share :
Baada ya kupangwa na timu za Norway na Senegal kwenye kundi Moja la fainali za kombe la Dunia 2026 huko Amerika ya Kaskazini Juni mwakani, kocha wa Ufaransa Didier Deschamps,amesema hilo ni moja ya makundi magumu.
Mbali na timu hizo bado mshindi mmoja wa mechi za mchujo wa mabara (Bolivia, Iraq, au Suriname) ataongezeka kwenye kundi hilo la I.
Baada ya hafla hiyo ya upangaji makundi mjini Washington DC, Didier Deschamps alitoa mtazamo wake wa awali."Ni kundi lenye nguvu, lenye ushindani.
Bado hatujamfahamu mpinzani wetu wa mwisho, lakini kwa Senegal na Norway, ni wazi kuwa Kundi I ni moja ya makundi magumu zaidi, kama sio magumu zaidi. Ni Kombe la Dunia, tunajua nini cha kutarajia. Sasa, tuna majibu. Tunajua wapinzani wetu wawili, tarehe za mechi, ingawa bado viwanja, ingawa kwa ujumla tushapafahamu kule tutakapocheza. "Alisema Deschamps.
Timu ya Taifa ya Norway ina Nyota wao Mshambuliaji wa Manchester City Erling Haaland ambaye alifunga mabai 16 katika mechi 8 za kufuzu.
Lakini Senegal Wawakilishi wa Afrika bado wana mtu kama Sadio Mane aliyewahi kutwaa kombe la Afrika akiwa na nchi yake lakini ubingwa wa Ulaya na Uingereza akiwa na klabu ya Liverpool.
Ufaransa yenyewe ina Kylian Mbappe ambaye alishinda kombe la Dunia 2018 akiwa na kikosi hicho cha The Blues na hadi sasa anadai goli mbili kuweka rekodi ya ufungaji kwa nchi yake akiwa na umri wa miaka 26.





