Kocha wa Ujerumani ang'aka ratiba ya FIFA.
Joyce Shedrack
June 26, 2026
Share :
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Ujerumani, Julian Nagelsmann, ameikosoa vikali ratiba ya Kombe la Dunia ya FIFA, akidai kuwa mfumo wa mashindano unaziweka timu zinazomaliza kileleni mwa makundi katika hali ya hasara kutokana na muda mdogo wa maandalizi kuelekea hatua ya mtoano.

Ujerumani ilimaliza nafasi ya kwanza katika Kundi E baada ya kukusanya pointi 6 na kuhakikisha kufuzu kabla ya kumalizika kwa mechi za makundi.
Hata hivyo, mabingwa hao mara nne wa dunia bado hawajafahamu watakaokutana nao katika hatua ya 32 bora, hadi pale mechi kadhaa za makundi zitakapokamilika baadaye wiki hii.
Kuchelewa huko kunamaanisha kuwa timu ya benchi la ufundi pamoja na kitengo cha uchambuzi wa mchezo wana muda mfupi sana wa kuandaa mbinu dhidi ya wapinzani wao watakaokutana nao katika mchezo wa mtoano utakaochezwa Boston tarehe 29 Juni.
Nagelsmann amesema hali hiyo inawafanya viongozi wa makundi kuwa katika mazingira magumu zaidi, licha ya kufanya vizuri katika hatua ya awali ya mashindano.
“Sidhani kama ni jambo zuri kwamba unakuwa kama unaadhibiwa kwa kuongoza kundi. Mimi si mpenzi mkubwa wa mfumo huu. Mtu yeyote anaweza kufikiria kuwa kuna njia bora zaidi kuliko kukaa usiku kucha Jumamosi ukichambua video za mechi, halafu unawasilisha mpinzani kwa wachezaji Jumapili,” alisema Nagelsmann akizungumza na waandishi wa habari.





