Kocha wa Yanga ataka umakini kwa wachezaji wake kuelekea mechi ya kesho.
Joyce Shedrack
April 10, 2026
Share :
Kocha Mkuu wa Yanga Pedro Goncalves, amesema kikosi chake kinatarajia mchezo mgumu dhidi ya TMA utakaochezwa kesho kwenye dimba la KMC Complex.
Akizungumza na waandishi wa habari, Goncalves kuelekea mchezo huo wa Kombe la Shirkisho amesema TMA ni timu inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza na kwa sasa inapitia kipindi kigumu ikijaribu kujinasua na hali hiyo, huku akibainisha kuwa hata Yanga yenyewe imekuwa katika kipindi cha changamoto msimu huu.
Kocha huyo amesisitiza kuwa mchezo huo wa Kombe ni tofauti na ligi, kwani huamuliwa ndani ya dakika 90 pekee, tofauti na mfumo wa alama wa msimu mzima. Amesema hali hiyo hufanya michezo ya FA Cup kuwa ya kusisimua zaidi kwa kuwa kila timu huingia ikiwa na matumaini ya kufanya makubwa.
Akirejea mchezo wao wa awali dhidi ya Cosmopolitan, Goncalves amesema ulikuwa ni mchezo mgumu licha ya ushindi walioupata. Ameeleza kuwa wapinzani wao walionyesha kiwango kizuri kisichokuwa na tofauti kubwa na baadhi ya timu za Ligi Kuu, jambo lililowalazimu kupambana kwa nguvu tangu mwanzo wa mchezo.
Amesema uzoefu wa mchezo huo umekuwa fundisho muhimu kwa kikosi chake, baada ya kukumbana na upinzani mkali uliowaweka katika wakati mgumu.





