"Kuitambua Palestina ni sawa na kuupa ushindi ugaidi" - Netanyahu
Eric Buyanza
February 17, 2024
Share :
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameupinga mpango wa kuitambua Palestina kama taifa huru kwa hoja kwamba uamuzi huo "utakuwa ni sawa na kuupa ushindi ugaidi.
Wizara ya mambo ya nje ya mamlaka ya Palestina imesema kutambuliwa kwa Palestina kama taifa huru sio zawadi au upendeleo kutoka kwa Netanyahu bali ni haki ya msingi iliyowekwa na sheria ya kimataifa.
Kauli ya Netanyahu ya kupinga kuitambua Palestina kama taifa huru pia imetolewa na mawaziri wenye ushawishi wa siasa kali za mrengo wa kulia Itamar Ben-Gvir na Bezalel Smotrich, ambao wamejibu ripoti iliyochapishwa na gazeti la Marekani la The Washington Post juu ya mpango wa kuitambua Palestina kama taifa huru.
Ripoti ya The Washington Post, iliyowanukuu wanadiplomasia kadhaa wa Marekani na mataifa ya Kiarabu imeeleza kuwa mshirika mkuu wa Israel, Marekani, inashirikiana kwa karibu na mataifa ya Kiarabu juu ya mpango madhubuti wa amani na wa muda mrefu kati ya Israel na Palestina.
Mpango huo, kando na mambo mengine, unajumuisha pia kuanzishwa kwa taifa huru la Palestina.
Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ameeleza kuwa, Israel inapinga kwa dhati "maagizo ya kimataifa" kuhusu suluhu ya kudumu katika mzozo wake na kundi la Hamas. Ameongeza kuwa, makubaliano ya amani yanaweza kufikiwa kwa njia ya mazungumzo ya moja kwa moja tu na bila ya masharti yoyote.
Naye Waziri wa fedha Bezalel Smotrich, anayeishi katika makaazi ya walowezi wa Kiyahudi kwenye ukingo wa magharibi, amesema taifa huru la Palestina litakuwa tishio kwa uwepo wa Israel. Suluhu ya mataifa mawili imekuwa sera kuu ya mataifa ya Magharibi katika kusuluhisha mgogoro wa muda mrefu kati ya Israel na Palestina.
DW