Kumfukuza Carrick hakutibu donda la Man U, INEOS wabebeshwa zigo
Eric Buyanza
September 19, 2026
Share :
Klabu ya Manchester United imetahadharishwa rasmi kuwa mpango wowote wa kumfukuza kocha wao mkuu, Michael Carrick, hautasaidia kutatua mgogoro na mfululizo wa matokeo mabovu yanayoikabili timu hiyo kwa sasa.
Tahadhari hiyo imekuja kufuatia ripoti ya hivi karibuni kutoka vyombo vya habari vya Uingereza, ikidai kuwa matatizo ya mashetani hao wekundu yapo juu zaidi ya benchi la ufundi, huku uongozi wa INEOS ukilaumiwa kwa kufanya makosa makubwa ya kimkakati kwenye dirisha la usajili la majira ya kiangazi yaliyopita.
Wachambuzi wa soka na wachezaji wa zamani wa klabu hiyo, akiwemo mshambuliaji wa zamani Louis Saha, wamesisitiza kuwa hata kama United itamleta kocha wa timu ya taifa ya Marekani Mauricio Pochettino au fundi wa Real Madrid Carlo Ancelotti, hakuna kitakachobadilika chini ya muundo wa sasa wa timu. Tatizo kubwa linaonekana kuwa ni uamuzi wa INEOS kushindwa kuziba nafasi muhimu zenye mapungufu kikosini.
Saha amebainisha kuwa, ingawa klabu hiyo ilisajili viungo watatu wapya, walifanya makosa makubwa kwa kutomtafuta mbadala sahihi wa kiungo mkongwe Casemiro, ambaye alikuwa nguzo muhimu msimu uliopita. Ukosefu wa usawa katika maeneo ya ulinzi na ushambuliaji umemwacha Carrick akiwa hana silaha za kutosha kukabiliana na ushindani.






