Kuwaona Al Ahly kwa Mkapa buku 5 tu
Sisti Herman
March 20, 2024
Share :
Meneja wa idara ya habari na mawasiliano wa klabu ya Simba Ahmed Ally leo amezindua hamasa na kutangaza viingilio kwaajili ya mchezo wa kwanza wa robo fainali ya ligi ya mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly utakaochezwa kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa machi 29.
“Hii leo tumamua kufanya mkutano na wanahabri kwenye Tawi la Simba la Feri hapa sokoni ikiwa ni maalumu na ikiwa kwa mara ya kwanza. Lengo letu ni kufikisha ujumbe tunaokusudia kwamba mechi hii ni kwa ajili ya mashabiki.”
“Wanasimba watambue kwamba tunawahitaji sana katika mchezo wa Ijumaa dhidi ya Al Ahly wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.”
“Kikosi chetu kiliondoka jana jioni kuelekea visiwani Zanzibar kwa ajili ya kuweka kambi ya siku nane ya kujiandaa na mechi hii dhidi ya Al Ahly. Dhumuni la kwenda Zanzibar ni mapendekezo ya mwalimu Benchikha kuhitaji utulivu wa hali ya juu na kufanya mazoezi mara mbili kwa siku ili kutengeneza timu ya kutoa ushindani.”
“Lakini pia mwalimu alihitaji kufanya mazoezi usiku, muda ambao mchezo utachezwa ili wachezaji kuzoea mazingiza ya usiku. Kikosi kitakuwa huko hadi wiki ijayo kitakaporudi kwa ajili ya mchezo huo.”
“Wengi walitamani mchezo uchezwe saa 10 jioni lakini mechi hizi zinapangwa na watu wengi kwa maslahi ya wengi wakiwepo wenye haki za matangazo na CAF wanaangalia mustakabali wa timu zote mbili. Lakini maslahi mapana ya watu wa imani zote yamezingatiwa na ndio maana ikapangwa muda wa saa 3 usiku ili kila timu na mashabiki wawe katika nafasi nzuri.”
“Kwa ukubwa tuliokuwa nao hivi sasa hatuna wasiwasi na muda wowote wa mechi ambao tutapangiwa, sisi tuko tayari kucheza katika muda wowote na kupata matokeo. Kwa maandalizi tunayofanya tunakwenda kufanya vizuri. Mkulima hachagui jembe.”
“Niwakumbushe tu Wanasimba hii sio mara ya kwanza kucheza mechi usiku, tulicheza dhidi ya USGN muda wa saa 4 usiku na tukamfunga. Kwa maandalizi tunayofanya InshaAllah tunakwenda kupata matokeo.”
“Hakuna Mwanasimba ambaye anashindwa kwenda uwanjani saa 3 usiku kuangalia Simba yake. Mwanasimba wa kweli, mwenye mapenzi na timu yake, abayetaka kuipeleka timu yake nusu fainali hawezi kushindwa kwenda uwanjani saa 3 usiku. Hakuna Mwanasimba wa hivyo.”- Ahmed Ally.
"Viingilio vya mchezo ni;
Mzunguko - Tsh. 5,000
Machungwa - Tsh. 10,000
VIP C - Tsh. 20,000
VIP B - Tsh. 30,000
VIP A - Tsh. 40,000
Platinum - Tsh. 200,000
Tanzanite - Tsh. 250,000
Tunaamini viingilio hivi ni rafiki kwa kila Mwanasimba."
"Nichukue nafasi hii kwa unyenyekevu kuwakaribisha na kuwaita Uwanja wa Mkapa siku ya tarehe 29. Ni mechi ambayo inatuhusu sana mashabiki wa Simba. Tumecheza mechi nyingi ya robo fainali lakini hii ndio robo fainali bora zaidi. Yani kama hauji kuona mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly jiulize mechi gani utakuja uwanjani."