Lawi kutua Azam FC ni suala la muda tu
Sisti Herman
July 1, 2025
Share :
Tetesi za usajili kutoka vijiwe vya soka zimeripoti kuwa Azam FC ni kama imepindua dili la vigogo waliokuwa wakimsaka beki wa Coastal Union, Lameck Lawi baada ya kuelezwa kwamba imetia mkono na kumalizana na beki huyo wa kati ili avae uzi wa Wanalambalamba kwa msimu wa 2025-2026.
Mmoja wa viongozi wa timu hiyo akizungumza, amesema ni kweli mchezaji huyo tayari ameshatia saini mkataba wa kuichezea Azam kwa miaka miwili kuanzia msimu ujao.
Awali, Simba msimu uliopita ilitangaza kumsajili Lawi kwa mkataba wa miaka mitatu, lakini mambo hayakuenda sawa dhidi ya timu iliyokuwa inammiliki (Coastal) hadi ikafikia hatua ya kupelekana Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Taarifa kutoka Azam zinaeleza lengo la kumsajili Lawi ambaye atakwenda kupambania namba na mabeki wa kigeni Yeison Fuentes kutoka Colombia na Yoro Diaby ni kuongeza nguvu kama mzawa.
Kwa beki mzawa anayecheza nafasi hiyo Azam ni Abdallah Kheri aliyekuwa anacheza Pamba kwa mkopo, ambapo uongozi utatathmini alichokifanya kama kinaweza kikaongeza nguvu au la.