Leo ni leo droo ya robo fainali CAF, nani kuceza na Simba na Yanga
Sisti Herman
March 12, 2024
Share :
Droo ya hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika inatarajiwa kuchezeshwa leo kuanzia saa 10:00 jioni kwa muda wa Afrika Mashariki, huko Cairo, Misri, huku Tanzania ikiweka rekodi.
Timu mbili zinazoiwakilisha Tanzania kwenye mashindano hayo, Yanga na Simba zitafahamu wapinzani wao rasmi katika hatua ya robo fainali kupitia droo hiyo ambayo itaendeshwa na kusimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Tanzania inaweka rekodi hapa ya kuwa nchi pekee ambayo timu zake mbili zinasubiri nani wa kukutana naye, lakini kikanuni haziwezi kukutana pamoja hapa labda nusu fainali.
Kutakuwa na vyungu viwili katika uchezeshaji wa droo hiyo ambapo cha kwanza kitakuwa na timu nne ambazo zimemaliza katika nafasi ya pili kwenye makundi yao wakati nyingine nne zitakuwa katika chungu cha pili ambacho kina timu zilizomaliza zikiwa kinara kwenye makundi yao.
Chungu cha kwanza kitakuwa na timu za Simba, Yanga, Esperance na TP Mazembe zilizomaliza za pili wakati chungu cha pili kikiwa na Al Ahly, Petro Luanda, Mamelodi Sundowns na Asec Mimosas.
Kwa kushika nafasi ya pili kwenye kundi B, Simba inaweza kupangwa na mojawapo kati ya Mamelodi Sundowns, Al Ahly au Petro Luanda wakati Yanga iliyomaliza ikiwa nafasi ya pili kwenye kundi D inaweza kukutana na ama Petro Luanda, Mamelodi Sundowns au Asec Mimosas.