"Leseni ya Mohamed Damaro inasoma kama mchezaji Mtanzania"Injinia Hersi.
Joyce Shedrack
April 11, 2026
Share :
Rais wa klabu ya Yanga Injinia Hersi Said, ameweka wazi kuhusu sakata la usajili wa kiungo wao Mohamed Damaro, akisisitiza kuwa mchezaji huyo si raia wa Guinea bali ni Mtanzania.
Akizungumza na TBC siku ya leo Hersi amesema leseni ya Damaro pamoja na mfumo wa usajili wa FIFA (TMS) vinamtambua kama Mtanzania, hivyo kusajiliwa kwake hakukiuki kanuni zozote.

“Leseni ya Damaro inasoma kama mchezaji mtanzania tangu Januari 2025. Sisi tukimtazama kwenye mfumo ambao FIFA wanautambua (TMS) mfumo unamtambua kama mchezaji wa Kitanzania. Kwahyo sisi kama Yanga ukituingiza kwenye hilo sakata unatukosea.”Injinia Hersi.
Ameeleza kuwa Damaro alitoka Singida Black Stars kama mchezaji wa ndani, na kuongeza kuwa madai yanayoikosoa Yanga kuvunja taratibu za usajili hayana msingi na yanapotosha ukweli.
Ikumbukwe kuwa hivi karibuni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba Crescentius Magori aliweka wazi kuwa wameomba ‘review’ kwa TFF kuhusu sakata hilo na baada ya hapo watasonga mbele kwenye mahakama ya michezo CAS na hata FIFA.





