Liverpool, Man U vitani kuwania saini ya Felix Nmecha wa Dortmund
Eric Buyanza
October 20, 2026
Share :

Sakata la usajili barani Ulaya limezidi kushika kasi huku miamba miwili ya Ligi Kuu ya England, Liverpool na Manchester United, ikiripotiwa kuingia kwenye vita kali ya kuwania saini ya kiungo nyota wa Borussia Dortmund na timu ya taifa ya Ujerumani, Felix Nmecha.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 26 amekuwa muhimili mkubwa katika safu ya viungo ya miamba hiyo ya Bundesliga, hatua inayomfanya kuwa miongoni mwa wachezaji wanaowaniwa kwa karibu na vitengo vya maskauti wa usajili nchini Uingereza.
Taarifa kutoka vyanzo mbalimbali vya michezo Ulaya zinaeleza kuwa Man United tayari wamefanya mawasiliano ya awali ili kuchunguza uwezekano wa kumnasa mchezaji huyo, wakitaka kuongeza nguvu na upana kwenye eneo lao la kiungo. Kwa upande wao, Liverpool wanamtazama Nmecha kama mbadala sahihi iwapo watashindwa kufikia makubaliano na klabu ya Bournemouth kwa ajili ya kumsajili nyota wao, Alex Scott.
Nmecha si mgeni na soka la Uingereza, kwani alilelewa katika akademia ya vijana ya Manchester City kwa zaidi ya muongo mmoja kabla ya kuhamia nchini Ujerumani. Hali hii inatajwa kuwa chachu inayoweza kumfanya arejee kwenye Ligi Kuu ya England (EPL).





