Liverpool wachomoa mpango wa Barcelona kumnunua Luis Díaz
Eric Buyanza
June 6, 2025
Share :
Liverpool wamekataa mpango wa Barcelona kumnunua Luis Diaz, mchezaji wa kimataifa wa Colombia mwenye umri wa miaka 28 ambaye amebakiza miaka miwili kwenye mkataba wake.
Akizungumza katika mkutano na wanahabari siku ya Alhamisi kabla ya pambano la Colombia dhidi ya Peru, Díaz alithibitisha ana furaha kubakia Liverpool, ingawa yuko makini kutathmini chaguo lake msimu huu.
"Ni wazi nina furaha sana Liverpool. Nimekuwa nikisema hivyo kila mara. Tangu siku ya kwanza nilipowasili nilipokelewa vyema. Kwasasa tuko kwenye mazungumzo, hii ni kawaida kwa sababu soko la uhamisho liko wazi na tunajaribu kuona ni nini kinachofaa zaidi kwetu," alisema Díaz.
"Nasubiri tu kuona nini kitakachofanyika. Ikiwa Liverpool watanipa mkataba mzuri wa kuongezwa au kama nitalazimika kukaa kwa miaka miwili niliyobaki nayo, nitafurahi na kuridhika. Yote inategemea na wao. Niko hapa kuamua na kuona ni nini kinachofaa kwetu na maisha yangu ya baadaye."
Díaz, aliyesajiliwa kwa pauni milioni 37.5 kutoka FC Porto Januari 2022, amekuwa mchezaji muhimu kwenye mafanikio ya Liverpool msimu huu.