M23 waudhibiti mji wa Shasha mashariki mwa Kongo!
Eric Buyanza
February 6, 2024
Share :
Hofu inaongezeka katika baadhi ya maeneo katika wilaya ya Masisi huko Kivu kaskazini, baada ya waasi wa M23 kutangaza kwamba wameudhibiti mji mdogo wa Shasha unaoiunganisha miji ya Goma na Bukavu.
Hali ni tete katika mji mdogo wa Shasha ambao ni muhimu kwa sababu ni mji unaounganisha miji ya Goma na Bukavu. Kulingana na vyanzo vya ndani, siku ya Jumamosi waasi wa M23 waliuteka mji huo baada ya mapigano makali kati yao na jeshi la kongo.
Wakati huo huo, mji wa Minova ulioko kusini mwa eneo hilo unawapokea mamia ya wakimbizi wa ndani wanaokimbia kutokana na waasi wa M23 kusonga mbele. Lakini hadi sasa watu hao wamekosa malazi na chakula, kama anavyo bainisha raia mmoja kwa njia ya simu.
"Tangu jumapili barabara inayoelekea Goma imefungwa baada ya M23 kudhibiti mji wa Shasha hali iliyowapelekea wengi wa raia kukimbia nakuwasili hapa Minova. Hali ni mbovu hapa Minova sababu mji wa Minova umewapokea wakimbizi wengi jambo linalotatiza hali ya kiuchumi na kuwa changamoto kubwa. "
Mapigano hayo yanayaosambaa yamekatisha shughuli za usafiri kwenye eneo hilo ambalo ni njia muhimu kwa usambazaji wa bidhaa. Waasi wa M23 wachukua udhibiti wa mji wa kimkakati karibu na Goma
Asubuhi ya Jumatatu (Tarehe 5 Feb), wananchi katika wilaya hiyo wamesema wameona misururu ya magari ya kijeshi inayoelekea kwenye eneo la mapigano huku wanajeshi wa serikali wakionekana tena kando ya mji huo wa Shasha baada ya wapiganaji wa M23 kurudi nyuma vimeelezea vyanzo hivyo vya kiraia.
Pascal Kulimushi ni mwakilishi katika bunge la vijana mjini Sake kilometa 15 kutoka eneo linaloshuhudia machafuko anaeleza.
"Muda huu tumeambiwa kwamba adui ameondoka Shasha na Kirotshe lakini huenda wamejificha ndani ya nyumba za raia au amerudi milimani. Raia wa kijiji cha Bweremana pia Kituva walilazimika kukimbia sababu ya mapigano ya hapo Nyamubingwa na kwenye mji mdogo wa Renga ".
Wiki chache zilizopita, baadhi ya mataifa ya magharibi ikiwemo Marekani kupitia waziri wake wa mambo ya nje Anthony Blinken, wameongeza shinikizo kwa serikali ya Kongo kufanya mazungumzo na kundi hilo la wapiganaji wa M23 lakini Kinshasa imeendelea kutupilia mbali agizo hilo huku waasi wa M23 wakisonga mbele kuviteka vijiji.
Hadi mchana wa jana makundi ya vijana wazalendo wanaoungwa mkono na jeshi la serikali ya Kongo, wameendelea kuzilenga kwa makombora ngome za waasi wa M23 kwenye milima katika mji huo mdogo wa SHASHA ambamo raia wameukimbia.