MAAJABU: Mlemavu wa macho aendesha gari kilomita 240 Uingereza
Eric Buyanza
September 25, 2026
Share :

Katika tukio ambalo liwameshtua wengi nchini Uingereza, mwanamume aliyetambulika kwa jina la Anthony Hall, mwenye umri wa miaka 50 ambaye ana ulemavu wa macho na hana leseni ya udereva, amekiri kuendesha gari la mpenzi wake umbali wa kilomita 240 huku akiwa amelewa chakari kabla ya kukamatwa na polisi.
Licha ya changamoto hiyo kubwa ya kimwili na kutokuwa na leseni kabisa, Hall alichukua funguo za gari la mpenzi wake usiku wa manane baada ya wawili hao kugombana na kuingia kwenye barabara kuu akisafiri asikokujua.
Mbinu aliyotumia Hall kuendesha gari hilo imewaacha wengi vinywa wazi. Aliiambia mahakama kuwa, ingawa haoni vizuri, ana uwezo wa kutofautisha mwanga hafifu. Ili kufanikisha safari hiyo aliamua kufuata kwa karibu taa nyekundu za nyuma za malori makubwa ya mizigo yaliyokuwa yakisafiri mbele yake. Cha kushangaza zaidi, alisimama njiani katika kituo cha huduma na mhudumu mmoja alimsaidia kujaza mafuta kwenye gari hilo bila hata kugundua kuwa dereva alikuwa na ulemavu wa macho.
Safari yake ya hatari ilifikia kikomo karibu na mji wa Carlisle baada ya polisi kupata taarifa kutoka kwa madereva wengine kuhusu gari lililokuwa likiyumba na kuhama njia mara kwa mara. Polisi walipomkamata na kumpima, waligundua kiwango chake cha pombe kilikuwa juu sana kuliko kiwango kinachoruhusiwa kisheria.
Hall amepigwa marufuku kuendesha gari na kuamriwa kupatiwa matibabu ya kisaikolojia na ya kuacha pombe.





