Mabaki ya panya yakutwa kwenye mkate 'maarufu' nchini Japan
Eric Buyanza
May 10, 2024
Share :
Kampuni maarufu ya utengenezaji wa mikate nchini Japan, imeagiza kurejeshwa kiwandani kwa maelfu ya mikate na wateja kurejeshewa pesa zao baada ya mabaki ya panya kukutwa kwenye baadhi ya mikate.
Takriban mifuko 104,000 ya mikate mweyeupe (white bread) inayotengenezwa na kampuni ya Pasco iliondolewa sokoni baada ya mikate miwili kukutwa ikiwa na mabaki ya panya.
Mkate wa Pasco ni chakula kikuu katika nyumba nyingi za kijapani na unapatikana kila mahali katika maduka makubwa na madogo kote nchini humo.
Hakuna ripoti hadi sasa za mtu yeyote aliyeugua kutokana na tukio hilo, Pasco ilisema katika taarifa yake kwa umma mapema wiki hii.
"Tunaomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza kwa wateja wetu, washirika wa kibiashara na pande zote zinazohusika," ilisema.
Pasco haikueleza ni namna gani mabaki ya panya yalivyoingia kwenye mikate yao, na kuahidi kufanya jitihada za kuongeza umakini ili jambo hilo lisijirudie tena.