Maelfu waondoka Afrika Kusini kukimbia vurugu za leo
Eric Buyanza
June 30, 2026
Share :

Maelfu ya raia wa kigeni wanaendelea kuondoka nchini Afrika Kusini huku hali ya taharuki ikiongezeka kuelekea maandamano dhidi ya wahamiaji yaliyopangwa kufanyika hii leo.
Maandamano hayo yamezua hofu kubwa miongoni mwa wageni, wengi wao wakisema wanalazimika kuondoka katika mazingira magumu na yasiyo na uhakika.
Baadhi ya wahamiaji wamesema wamechukua uamuzi wa kurejea nchini mwao kutokana na kuhofia usalama wao, huku wengine wakilazimika kuacha jamaa zao nyuma kutokana na hali ya dharura inayowakabili.
Katikati mwa mji wa Durban, makundi ya watu yalionekana yakisimamisha raia wanaodhaniwa kuwa wageni, kuwafanyia upekuzi na kukagua nyaraka zao za utambulisho—hatua iliyoongeza wasiwasi kuhusu uwezekano wa baadhi ya watu kujichukulia sheria mkononi.
Kutokana na hali hiyo, mamlaka za Afrika Kusini zimesema zimeimarisha usalama na ziko tayari kukabiliana na tukio lolote la uvunjifu wa amani litakalojitokeza.
Waziri Mkuu wa jimbo la KwaZulu-Natal Thami Ntuli, amesema kumeongezwa idadi ya maafisa wa usalama katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo ili kuhakikisha hali ya utulivu na kwamba raia wote, wakiwemo waandamanaji na wageni, watalindwa.
DW





