Magari mkweche marufuku kuingia stendi mpya ya Mwenge
Eric Buyanza
February 3, 2024
Share :
Wakati wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam wakisubiri kwa hamu kufunguliwa kwa Stendi ya Mabasi Mwenge, uongozi wa Wilaya ya Kinondoni umesema haitaruhusu magari mabovu kuingia katika kituo hicho.
Akizungumza na kituo cha Radio One, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, alisema kituo hicho kitakapoanza kitaruhusu kuingia kwa magari yaliyosajiliwa na yenye ubora uliothibitishwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA).
“Kwa hiyo tutaruhusu magari yaliyosajiliwa kuingia katika kituo hicho, hatutaruhusu gari lolote liingie, magari ambayo ni bora na yenye uimara, na ni utaratibu wa kawaida hata Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani wanasimamia,” alisema
Alisema uongozi wa wilaya ya Kinondoni unatamani kuwe na magari mazuri yanayoingia katika stendi hiyo, si gari linaiongia pale linaanza kumwaga mafuta bali liwe vizuri.
“Tutasimamia ubora wa majengo, biashara na huduma zingine zitakazohitajika. Gari ambalo halitakuwa na sifa hizo yanyooshe tu yaelekee kwingineko yasiingie katika kituo hicho,” alisema.