Mahakama yathibitisha CAG Prof. Assad aliondolewa kimakosa
Sisti Herman
October 8, 2026
Share :

Baada ya miaka saba Mahakama ya Rufani ya Tanzania hatimaye imeweka nukta na kuthibitisha rasmi kuwa hatua ya kumwondoa madarakani aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Juma Assad, mnamo Novemba 2019, ilikuwa ya kimakosa na kinyume kabisa cha Katiba ya Nchi.
Hukumu hiyo iliyosomwa na Jaji Sehel kwa niaba ya jopo la Majaji watano waliosikiliza Rufaa ya Madai Namba 176 ya Mwaka 2023 jana, Oktoba 6, 2026 imebainisha kuwa Ofisi ya CAG ilivunjiwa heshima na ulinzi wake wa kikatiba pale Mamlaka ya Uteuzi ilipomtengua Prof. Assad kabla ya kufikisha umri wa kustaafu wa miaka 65.
Shauri hilo lililofunguliwa na mwanasiasa Zitto Zuberi Kabwe, lilikuwa likipinga Kifungu cha 6(1) cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma (PAA) cha Mwaka 2008 kilichotumiwa na Serikali kuweka ukomo wa miaka mitano wa kuhudumu kwa CAG.Kwenye uamuzi huo wa kihistoria, Mahakama ya Rufani imetamka wazi kuwa Bunge halina mamlaka ya kutunga sheria yoyote inayopunguza kinga na ulinzi wa ajira aliopewa CAG ndani ya Ibara ya 144(1) ya Katiba.
Mahakama imesisitiza kuwa CAG anaweza kuondolewa madarakani kwa njia mbili tu: kufikisha umri wa miaka 65 ya kustaafu au kupitia Tume Maalum (Tribunal) pindi anaposhindwa kutekeleza wajibu wake au kupoteza sifa.





