Majenerali wawili washtakiwa DRC kwa kukimbia vita na kumuachia mji adui
Eric Buyanza
September 26, 2026
Share :

Mahakama Kuu ya Kijeshi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imefungua rasmi kesi ya kihistoria inayowakabili majenerali wawili wa ngazi za juu wa jeshi la serikali (FARDC), wanaotuhumiwa kwa makosa ya uoga na kudhoofisha ari ya askari kufuatia kuanguka kwa mji wa kimkakati wa Bukavu mikononi mwa waasi wa AFC/M23 mnamo Februari 2025.
Maafisa hao waliofikishwa mahakamani chini ya ulinzi mkali wakitokea gerezani ni Jenerali-Major Robert Yav Avul (aliyekuwa mkuu wa kanda ya 33 ya kijeshi) na Jenerali wa Kikosi André Ehonza Uketi (aliyekuwa mkuu wa operesheni za Sukola II Kusini mwa Kivu).
Kulingana na hati ya mashtaka iliyosomwa na msajili wa mahakama, Luteni-Kanali René Kiembi, viongozi hao wanakabiliwa na makosa yafuatayo:
Jenerali Robert Yav anashutumiwa kumuachia adui jiji la Bukavu bila kuonyesha upinzani wowote wa kijeshi baada ya maeneo ya Kalehe, Katana, na Kavumu kuanguka, ambapo alikimbilia Nyatende kisha Nyangezi.
Jenerali André Ehonza anashtakiwa kwa kuacha nafasi yake ya ulinzi huko Amsar usiku wa manane ili kumfuata Jenerali Yav, huku akidaiwa kuwatisha na kuwakatisha tamaa askari walio chini yake kwa kukuza mno uwezo wa kijeshi wa vikosi vya waasi.





