Mama afariki akimuokoa binti yake wakati ghorofa linaporomoka
Eric Buyanza
June 27, 2026
Share :

Katika tukio la kuhuzunisha mwanamke mmoja nchini Venezuela amepoteza maisha yake wakati akijaribu kumuokoa binti yake mchanga wakati wa tetemeko kubwa la ardhi.
Mwanamke huyo aliyetambulika kwa jina la Andrea Ruiz ni mke wa mchezaji wa mpira wa miguu nchini Venezuela, Héctor "Kike" Bello, anayechezea klabu ya Marítimo de La Guaira.
JINSI ILIVYOTOKEA
Wakati ghorofa lao lilipokuwa likiporomoka kutokana na tetemeko, Andrea alijitupa juu ya binti yake wa mwaka mmoja anayeitwa Alana ili kukinga mwili wa mtoto huyo dhidi ya vifusi vinavyoanguka.
Waokoaji walipofika eneo la tukio, walimkuta Andrea akiwa tayari ameshafariki huku mtoto akiwa hai akiwa chini ya mwili wa mama yake kutokana na kinga hiyo ya kishujaa.
Mtoto alikimbizwa hospitali kupata matibabu na anaendelea vizuri.
Mchezaji Héctor Bello ameweka ujumbe mzito wa majonzi kwenye mtandao wa Instagram akisema: "Nitamsimulia binti yetu hadithi ya jinsi ulivyookoa maisha yake, mpenzi wangu—jinsi ulivyotoa maisha yako kwa ajili ya binti yetu, jinsi ulivyokuwa mwanamke jasiri ambaye hukumwacha hata wakati unatoa pumzi yako ya mwisho."





