Mama wa kambo jela miaka 5 kwa kumchoma mtoto na maji moto
Eric Buyanza
June 12, 2025
Share :
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Geita imemhukumu mkazi wa Nyatorotoro, Janeth Emmanueli (20) kutumikia kifungo cha miaka mitano gerezani kwa kosa la kumchoma na maji ya moto kwenye makalio mtoto mvulana mwenye umri wa miaka mitatu na kumsababishia maumivu makali.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Buruno Bongole baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha kosa hilo pasipo kuacha shaka yoyote.
Hakimu Bongole alisema mahakama hiyo inatoa adhabu dhidi ya mshtakiwa huyo ili iwe fundisho kwake na kwa wanawake wengine wenye tabia ya kuwachoma na maji ya moto watoto wa kambo kama yake.
Alisema upande wa mshtaka ulikuwa ukiongozwa na Wakili wa Serikali Concessa Desideri ambaya alipeleka mahakamani mashahidi wanne na vielelezo vitatu ambavyo vilithibitisha mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo.
Hakimu Bongole alisema mtoto huyo alikuwa anaishi na mama wa kambo, Janeth, ambaye ni mshtakiwa katika maeneo ya Nyatorotoro wilaya ya Geita. Mshtakiwa huyo alikuwa anamtenda mtoto huyo vitendo vya kikatili mara kwa mara.
Alisema kuwa siku ya tukio hilo Agosti 18, 2024, huko Nyatorotoro wilayani Geita, mshtakiwa huyo alichemsha maji ya moto kisha kumchukua mtoto huyo na kumkaliza kwenye maji ya moto ndipo mtoto huyo aliungua makalio na kupata majeraha na maumivu makali.
Alisema kuwa baada ya tukio hilo, mwenye nyumba alikokuwa anaishi mshtakiwa huyo, alipiga simu Kituo cha Polisi Geita na askari walifika na kumchukua mtoto huyo kisha kumpatia Fomu Na. 3 ya Polisi (PF3) na kupelekwa Hospitali ya Wilaya ya Geita kwa matibabu. Mtoto alilazwa huko kwa siku tatu. Daktari aliyemfanyia uchunguzi alibaini kuwa mtoto huyo alikuwa anafanyiwa ukatili mkubwa, maana mwili mzima wa mtoto huyo ulikuwa na makovu ya kufinywa na makovu ya kupigwa kwa fimbo.
Hakimu Bongole alisema kuwa baada ya mtoto huyo kuruhusiwa kutoka hospitalini, alipelekwa kituo cha kulelea watoto waliofanyiwa ukatili cha Moyo wa Huruma cha Kanisa Katoliki.
Alisema mshtakiwa huyo alikamatwa na alipohojiwa kuhusiana na kosa hilo, alikiri kuhusika. Upelelezi wa kesi hiyo ulipokamilika, alifikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
NIPASHE