Marekani kufuta Viza za wanafunzi wa China
Eric Buyanza
May 29, 2025
Share :
Marekani imetangaza kuwa itaanza kufuta viza za wanafunzi kutoka China, hususan wale wanaohusishwa na Chama cha Kikomunisti cha China au wanaosomea fani zinazotajwa kuwa nyeti kwa usalama wa taifa.
Tangazo hilo limetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio siku ya Jumatano, ambaye pia amesema kuwa masharti ya viza yatapitiwa upya ili kuongeza uchunguzi kwa maombi kutoka China na Hong Kong.
Mpango huo unatajwa kuwa sehemu ya juhudi za utawala wa Rais Donald Trump za kuimarisha udhibiti wa uhamiaji.
China ilikuwa na idadi ya pili kwa ukubwa ya wanafunzi wa kimataifa waliokuwa wakisomea Marekani mwaka 2023/2024, wakiwa 277,398.
Hadi sasa, ubalozi wa China mjini Washington haujatoa kauli rasmi kuhusiana na tangazo hilo.
Wachambuzi wanasema hatua hii huenda ikaathiri uhusiano wa kielimu na kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili yenye mvutano wa muda mrefu.
DW