Marekani kutuma makombora Ujerumani kuikabili Urusi
Eric Buyanza
July 11, 2024
Share :
Marekani itaanza kupeleka makombora ya masafa marefu nchini Ujerumani kuanzia mwaka 2026, hatua muhimu inayolenga kudhibiti ongezeko la vitisho vya Urusi barani Ulaya.
DW inaripoti kuwa, chini ya makubaliano ya mataifa hayo yaliyotangazwa kwenye mkutano wa kilele wa NATO mjini Washington, Marekani itapeleka silaha nzito kabisa ambazo haijawahi kuzipeleka Ulaya tangu enzi ya Vita Baridi, likiwa ni onyo la wazi kwa Rais Vladimir Putin.
Taarifa yao ya pamoja ilisema maandalizi ya kupelekwa silaha hizo kwa awamu, ambazo ni pamoja na makombora ya masafa marefu, yanafanyika.
Hatua hiyo pengine ingezuiwa chini ya makubaliano ya Nyuklia kati ya Marekani na uliokuwa Umoja wa Sovieti ya mwaka 1987, yaliyovunjika mwaka 2019.
Kwenye mkutano huo, wakuu wa ushirika wa NATO aidha walikubaliana kuiongezea Ukraine msaada wa kijeshi wa karibu dola bilioni 40 mwaka ujao.