Marekani, Uingereza zaituhumu China kwa ujasusi mtandaoni
Eric Buyanza
March 26, 2024
Share :
Maafisa wa Marekani na Uingereza wamefungua mashitaka, kutangaza vikwazo, na kuituhumu China kwa kuendesha kampeni kubwa ya ujasusi wa mitandaoni, ujasusi ambao unadaiwa kuwakumba mamilioni ya watu wakiwemo wabunge, wasomi, waandishi habari na makampuni wakiwemo wanakandarasi wa sekta ya ulinzi.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Marekani Lisa Monaco amesema katika taarifa kuwa lengo la operesheni hiyo ya udukuzi wa kimataifa lilikuwa ni "kuwakandamiza wakosoaji wa utawala wa China, kuingilia taasisi za serikali na kuiba siri za biashara.
Maafisa mjini London wameituhumu APT31 kwa kuwadukua wabunge wa Uingereza wanaoikosoa China na kusema kuwa kundi la pili la majasusi wa China lilihusika na udukuzi wa taasisi ya mausala ya uchaguzi ya Uingereza na kuingilia data za mamilioni ya watu nchini humo.
Hata hivyo Ubalozi wa China mjini London uliyaita madai hayo kuwa ni ya "Kutungwa na ni kashfa zenye nia ovu kwa nchi yake."