Marekani yaitaja Kenya kitovu cha bidhaa bandia
Eric Buyanza
May 8, 2026
Share :

Ripoti ya Ofisi ya Mwakilishi wa Bishara ya Marekani-USTR imeitaja Kenya kuwa njia kuu ya kupitisha na kusambaza bidhaa bandia duniani, zikiwemo dawa, vifaa vya kielektroniki na nguo kutoka China na India hadi Afrika.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, bidhaa bandia zinazotoka hasa katika vituo vya uzalishaji kama China na India zinazidi kuingia katika masoko ya Afrika kupitia nchi zenye mifumo dhaifu ya kulinda haki miliki.
Kenya imetambuliwa kama soko la bidhaa hizo pamoja na njia ya kusafirisha bidhaa bandia kwenda mataifa mengine ya eneo hili.
Ripoti ya USTR inaonya kuwa biashara ya bidhaa bandia inaleta hatari kubwa kiuchumi na kiafya. Kwa mfano, dawa bandia zinaweza kuwa na kemikali hatari au kukosa vitu muhimu vya matibabu, huku vifaa vya kielektroniki na vipuri vya magari visivyo na ubora vikihatarisha usalama wa watumiaji.
Bidhaa nyingine ni kama vipodozi, nguo na viatu vya chapa maarufu, simu za bei rahisi na vifaa vya kielektroniki na bidhaa za nyumbani kama vifaa vya plastiki na vifaa vya umeme.
Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa biashara hiyo haramu inadhoofisha biashara halali, inapunguza mapato ya ushuru kwa serikali, inakatisha wawekezaji tamaa na kuimarisha mitandao ya kihalifu.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo bidhaa hizi huingia kupitia Bandari kuu ya Mombasa, viwanja vya ndege kama Jomo Kenyatta, mipaka ya nchi jirani Uganda, Tanzania, Somalia na Ethiopia.
Ripoti hiyo ya Marekani sasa inaongeza shinikizo kwa Kenya kuimarisha utekelezaji wa sheria za haki miliki, kuimarisha udhibiti mipakani na kuongeza uhamasishaji wa walaji ili kulinda biashara halali na kurejesha imani ya wawekezaji na washirika wa biashara.
DW





