Marekani yaiwekea vikwanzo Wizara ya Ulinzi ya Rwanda
Eric Buyanza
October 29, 2026
Share :

Serikali ya Marekani imetangaza vikwazo vikali vya kiuchumi dhidi ya Wizara ya Ulinzi ya Rwanda (MoD) pamoja na Benki ya Kijeshi ya nchi hiyo, Zigama Credit and Savings Society, kwa tuhuma za kuchochea machafuko na kufadhili makundi ya waasi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Hilo limetangazwa kupitia taarifa rasmi zilizotolewa kwa pamoja na Wizara ya Hazina ya Marekani (US Treasury) na Idara ya Uhusiano ya Kimataifa (Department of State).
Kwa mujibu wa Serikali ya Marekani, Wizara ya Ulinzi ya Rwanda imekuwa ikiongoza na kufadhili oparesheni za Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) ndani ya DRC, ambapo wanajeshi hao wanatuhumiwa kupigana bega kwa bega na waasi wa kundi la M23 pamoja na muungano wa AFC.
Kwa upande wa Benki ya Kijeshi ya Zigama, Marekani inadai kuwa taasisi hiyo imetumika kama nguzo kuu ya kifedha kurahisisha miamala ya mamilioni ya dola kwa ajili ya ununuzi wa zana za kivita, ikiwemo silaha na risasi kutoka China na mataifa mengine. Aidha, benki hiyo inatuhumiwa kusaidia utakatishaji wa fedha zinazotokana na biashara haramu ya usafirishaji wa madini ya dhahabu na coltan kutoka maeneo yanayodhibitiwa na waasi nchini DRC kwenda Kigali, Rwanda.
Waziri wa Fedha wa Marekani, Scott Bessent, amebainisha kuwa hatua hiyo imechukuliwa chini ya agizo la Rais Donald Trump. Amesema hatua hii ni shinikizo la kuilazimisha Rwanda kuwajibika kufuatia kile kilichotajwa kama ukiukwaji wa wazi wa makubaliano ya amani ya Washington Accords yaliyosainiwa Desemba 2025 kati ya viongozi wa Rwanda na DRC ili kumaliza uhasama.
Kufuatia uamuzi huo, mali zote na maslahi ya kifedha ya Wizara ya Ulinzi ya Rwanda na Benki ya Zigama yaliyopo ndani ya ardhi ya Marekani au yanayodhibitiwa na raia wa Marekani yamezuiliwa rasmi (frozen). Vilevile, raia na mashirika yote ya Marekani yamepigwa marufuku kufanya miamala au biashara yoyote na taasisi hizo zilizowekewa vikwazo.





