Marekani yasusia kutoa heshima kwa hayati Ebrahim Raisi
Eric Buyanza
May 31, 2024
Share :
Marekani imesusia kutoa heshima za Umoja wa Mataifa kwa Rais wa Iran Ebrahim Raisi siku ya Alhamisi (30.05.2024) ikisema alihusika katika matukio mengi ya ukiukwaji wa kutisha wa haki za binadamu.
Nante Evans, msemaji wa ujumbe wa Marekani katika Umoja wa Mataifa amesema Marekani haingehudhuria hafla hiyo ya kumuenzi Rais Raisi katika nafasi yoyote ile.
Nante alisema Raisi alihusika katika vitendo kadhaa vya kutisha vya ukiukaji wa haki za binadamu na unyanyasaji, ikiwa ni pamoja na mauaji ya maelfu ya watu kinyume cha sheria na wafungwa wa kisiasa mnamo mwaka 1988.
Msemaji huyo amesema baadhi ya matukio mabaya kabisa ya ukiukaji wa haki za binadamu kuwahi kurekodiwa yalifanyika wakati wa uongozi wake.
Ujumbe wa Iran katika Umoja wa Mataifa umekataa kutoa kauli kuhusu hatua ya Marekani.
Baraza kuu la Umoja wa Mataifa lenye wanachama 193 kwa kawaida hukutana kutoa heshima kwa kiongozi yoyote wa dunia ambaye alikuwa mkuu wa nchi wakati wa kifo chake.
DW