Marekani yatoa msamaha wa muda kwa mafuta ya Urusi
Eric Buyanza
March 14, 2026
Share :

Marekani imetoa msamaha wa siku 30 unaoruhusu mataifa kununua mafuta ghafi ya Urusi na bidhaa za petroli ambazo tayari ziko baharini licha ya vikwazo ilivyowekewa Urusi.
Uamuzi huo uliotangazwa na Waziri wa fedha Scott Bessent, unalenga kutuliza masoko ya nishati duniani ambayo yamevurugika pakubwa kutokana na vita vinavyoendelea kati ya Iran na washirika Marekani na Israel.
Msamaha huo unahusu mafuta yaliyopakiwa kwenye meli tarehe 12 mwezi Machi au kabla yake na utadumu hadi Aprili 11 saa sita usiku kwa saa za Marekani. Uamuzi wa kutoa msamaha umefanyika katika wakati ambapo masoko ya mafuta yametikiswa na mgogoro unaendelea Mashariki ya Kati.
Mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran yamesababisha kuvurugika kwa usafirishaji wa mafuta kupitia Mlango Bahari wa Hormuz, njia muhimu kwa karibu theluthi moja ya mafuta yanayosafirishwa duniani. Hali hiyo imesababisha bei za mafuta ghafi kupanda hadi zaidi ya dola 100 kwa pipa, japo bei zilianza kushuka kidogo masoko ya Asia baada la tangazo hilo la Marekani.
DW





