Marufuku Hospitali kufua nguo kwa mikono
Eric Buyanza
May 17, 2024
Share :
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), imepiga marufuku wafanyakazi katika hospitali na vituo vya afya nchini kufua nguo kwa mikono, badala yake imewataka watumie mashine ili kuwaepusha kupata maambukizi ya magonjwa.
Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, Dk. Rashid Mfaume, ametoa katazo hilo wakati akizungumza na waganga wakuu wa wilaya na wakuu wa idara za halmashauri za Mkoa wa Manyara.
Ametoa agizo hilo baada ya kutembelea Hospitali ya Mji wa Babati ya Mrara na kukuta uchafu katika maeneo ya Kituo cha Afya Daudi kilichopo katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu.
Amesema TAMISEMI haitakubali kuona wafanyakazi wanafua nguo kwenye vituo vya afya na hospitali kutumia mikono kwa kuwa wanaweza kupata magonjwa ya mlipuko.