"Mashabiki wanaopokea timu za wageni na kuzishabikia, tutadili nao" - Ndumbaro
Eric Buyanza
March 14, 2024
Share :
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Damas Ndumbaro amesema serikali itawachukulia hatua mashabiki wa Simba na Yanga wenye tabia ya kusapoti timu za wageni zinapokuja kucheza nchini.
Akiongea kwenye 'Space' ya Mwananchi kupitia ukurasa wa X (zamani Twitter), Waziri Ndumbaro amewataka mashabiki kuacha kuwapokea na wajue ya kwamba mechi hizi za robo fainali ni kufa na kupona na kinachotakiwa ni kuhakikisha timu zetu zinashinda.
"Wiki iliyopita tulitoa tamko, Serikali tunataka kukaa na Simba, Yanga na TFF, ili watuambie kama serikali, tunahitaji kutoa mchango gani ili timu kushinda robo fainali na ziingie nusu fainali. Tunaweza kukutana Jumanne wiki ijayo ili kupanga mikakati."
Kuhusu mashabiki amesema; "Watanzania niwaombe sana najua kuna utani wa jadi, lakini kwenye mechi hizi za robo fainali ni mechi za kufa na kupona, hatutegemei kuona Mtanzania yeyote akienda kupokea wageni uwanja wa ndege, ama kuvaa jezi za timu za wageni."
"Sisi kama Serikali hatutawaachia hili TFF wala Simba na Yanga, kwa hiyo tutahangaika na mtu ambaye tutaona ni msaliti. Tunaomba Watanzania watuelewe na watusamehe kwa sababu tunataka timu hizi zifanikiwe."
"Kwa hiyo wewe Mtanzania ambaye utaweka kimbelembele kwenda kupokea wageni uwanjani wa ndege, kuwasapoti kwa namna yeyote, hatutakuelewa na tutadili na wewe kwa vile ambavyo tunaona inafaa."
"Tumekuwa nchi pekee iliyofanikiwa kuingiza timu mbili mwaka huu, lakini ukishapata mafanikio haupaswi kutumia muda mwingi sana kushangilia hayo mafanikio, unatakiwa uangalie unafanya nini ili kuendelea kupata mafanikio zaidi."