Massanza na Pablo Almasi kimewalamba kisa mechi dhidi ya Simba.
Joyce Shedrack
September 4, 2026
Share :
Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), katika kikao chake kilichofanyika Septemba 3, 2026, imewatoza faini ya jumla ya Sh milioni 20 maafisa wawili wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Singida Black Stars.

Kamati hiyo imepitia mwenendo na matukio mbalimbali yaliyotokea katika Ligi Kuu ya NBC, ikiwemo mchezo namba 017 kati ya Singida Black Stars na Simba SC, uliomalizika kwa Simba SC kushinda mabao 2-1.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Singida Black Stars, Hussein Massanza, ametozwa faini ya Sh milioni 10 kwa kosa la kumshutumu na kumtukana mwamuzi wa kati wa mchezo huo kupitia chapisho moja la mtandaoni.
Kwa mujibu wa TPLB, kitendo hicho ni kinyume na Kanuni ya 49:3 na 49:4 ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti kwa Maofisa Habari wa Klabu, huku adhabu hiyo ikitolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 49:7.
Aidha, Pablo Almasi, ambaye ni Afisa kutoka Idara ya Habari na Mawasiliano ya Singida Black Stars, naye ametozwa faini ya Sh milioni 10.
Almasi ameadhibiwa kwa kusambaza machapisho kupitia ukurasa wake wa Instagram yaliyokuwa na maudhui ya kumkashifu mwamuzi wa mchezo kati ya Singida Black Stars na Simba SC, pamoja na kuikebehi teknolojia ya Football Video Support (FVS) iliyotumika katika mchezo kati ya Young Africans na Coastal Union.
TPLB imesema kitendo hicho ni kinyume na Kanuni ya 49:4 na 49:5 ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti kwa Maofisa Habari wa Klabu, huku adhabu hiyo pia ikitolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 49:7.





