pmbet

Maswali ya kimbinu waliyoulizana Luis Enrique na Arteta Fainali UCL 2026

Sisti Herman

May 31, 2026
Share :

 

Utangulizi

Klabu ya PSG ya Ufaransa imetwaa Ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA Champions League) baada ya kuifunga klabu ya Arsenal ya Uingereza kwa mikwaju ya penalti 4-3 kwenye mchezo wa fainali iliyomalizika hivi punde kwenye uwanja wa Puskas Arena jijini Budapest nchini Hungary.

Kwenye mchezo huo kulikuwa na burudani nyingi lakini kubwa zaidi ni ile vita ya mbinu kati ya makocha wa timu hizo Luis Enrique was PSG na Mikel Artata wa Arsenal, wote raia wa Hispania.

Vikosi vya timu zote mbili;


Luis Enrique na Mikel Arteta waliingia na vikosi hivi hapa chini;
 


Mbinu za makocha zilikuwaje?

Hivyo zilikutana timu bora kwenye nyakati mbili uwanjani na hilo lilidhihirika kwenye aina ya mbinu zilizotumiwa na makocha wa timu zote mbili.

Arsenal kwasababu ilikuwa timu bora kiuzuiaji, ilichagua kuzuiaji nyakati nyingi wakiwa na mfumo wa 4-4-2 huku PSG wakiwa wanamiliki mpira na mfumo wa 4-3-3, ambapo mifumo hii ilinyumbulika kwenye miundo tofauti kulingana na theluthi ya uwanja ambapo PSG wanamiliki mpira, Kama;

(i) Mpira ukiwa kwenye nusu ya PSG, Arsenal walizuia na muundo wa 4-2-4 ambapo;


- Havertz, Odegaard, Saka na Trossard walikuwa kwenye mstari wa mbele wa uzuiaji
- Rice na Lewis-Skelly walikuwa kwenye mstari wa kati wa uzuiaji
- Gabriel, Saliba, Hincapie na Mosquera walikuwa kwenye mstari wa nyuma wa uzuiaji


Huku PSG, Mpira ukiwa kwenye nusu yao, walijenga shambulizi na muundo wa 4-3-3, ambapo;

- Hakimi, Mendez, Marquinhos na Pacho wakiwa mbele ya Safonov
- Vitinha, Ruiz na Joao Neves wakiwa kwenye mbele ya mabeki na umbo la Single Pivot
- Kvaratshelia na Doue wakiwa pembeni ya Dembele kwenye mstari wa mbele

(ii) Mpira ukiwa kwenye theluthi ya kati na ya mwisho ya uwanja, Arsenal walizuia na muundo wa 4-4-2 ambapo;

- Havertz, Odegaard walibaki kwenye mstari wa mbele wa uzuiaji
- Saka na Trossard wakisogea usawa wa Rice na Lewis-Skelly kwenye mstari wa kati wa uzuiaji
- Gabriel, Saliba, Hincapie na Mosquera walikuwa kwenye mstari wa nyuma wa uzuiaji


Huku PSG, Mpira ukiwa kwenye theluthi ya kati na mbele, PSG walishambulia na muundo wa 3-2-5na 2-3-5, ambapo;

- Ikiwa 3-2-5, Mendez hubaki usawa wa Pacho na Marquinhos nyuma, Hakimi husogea usawa wa washambuliaji, huku Vitinha na Ruiz wakibaki mbele ya mabeki.
- Ikiwa 2-3-5, Mendez husogea usawa wa Vitinha na Ruiz wakati Hakimi akiwa usawa wa washanbuliaji.

(iii) Kuna nyakati pia mpira ukiwa kwenye theluthi yao ya mwisho, Arsenal walizuia na muundo wa 6-2-2, ambapo;


- Havertz, Odegaard walibaki kwenye mstari wa mbele wa uzuiaji
- Rice na Lewis-Skelly walibaki kwenye mstari wa kati wa uzuiaji
- Saka na Trossard wakisogea nyuma zaidi usawa wa Gabriel, Saliba, Hincapie na Mosquera walikuwa kwenye mstari wa nyuma wa uzuiaji

Maswali magumu ya kimbinu waliyoulizana Enrique na Arteta.

1. Mbinu za timu ipi zitatawala mchezo?

Ilikuwa ni mechi iliyokutanisha timu bora kwenye maeneo mawili uwanjani, timu bora zaidi kiushambuliaji msimu huu PSG dhidi ya timu bora zaidi kiuzuiaji msimu huu Arsenal.

Kwenye msimu huu wa UEFA Champions league, PSG ndiyo timu bora zaidi kiushambuliaji ikiwa imefunga goli 45 huku Arsenal ikifunga goli 30 tu.

Kwenye msimu huu wa UEFA Champions league, Arsenal ndiyo timu bora zaidi kiuzuiaji ikiwa imefungwa goli 7 tu, huku PSG ikifungwa goli 23.

Baada ya dakika 120 za mchezo, hizi zilikuwa takwimu za mchezo;

 


Takwimu zinaeleza wazi kuwa;

Licha ya PSG kutawala umiliki wa mchezo wa 75%, lakini haikuweza kutengeneza hatari nyingi kwenye lango la Arsenal ikiwa na mashuti manne tu yaliyolenga lango wakifunga goli 1 sawa na Arsenal waliomiliki mpira kwa 25% huku wakipiga shuti 1 tu lililolenga lango nalo ni goli

Hivyo kimbinu, Arsenal kutokana na mbinu zao za uzuiaji walikuwa na udhibiti wa mchezo zaidi kuliko PSG waliotawala umiliki wa mpira na kushindwa kutengeneza nafasi za kufunga.

2. Arsenal itakabiliana vipi na Presha ya PSG?


Kwenye msimu uliopita PSG ilirekodiwa kuwa ni timu inayoruhusu mpinzani kucheza idadi ndogo zaidi ya pasi Kabla haijapora mpira (PPDA - Passes Per Defensive Actions) ikiwa na wastani wa PPDA 8.5, sawa na kuruhusu wapinzani wao kucheza chini ya pasi 8 tu kabla hawajapora mpira.


Kukabiliana na hali hiyo, Arsenal walikuja na mkakati wa kutoanzisha mashambulizi kutoka nyuma kwa pasi fupi wakiwa na lengo la kuzuia PSG kutopora mipira yao mingi.

Mfano mzuri ni pasi nyingi kutoka kwa kipa wao David Raya zilikuwa pasi ndefu kuelekea kwenye nusu ya PSG lengo ni kutopoteza mpira Karibu na lango lao kuepuka makosa kutokana na shinikizo la PSG (PSG's High Pressing)
 


3. Arsenal inakabiliana vipi na mitego wa kushambulia wa PSG?

Kwasababu PSG ni timu bora kiushambuliaji ikiwa imefunga goli 45, Arsenal ilihitaji mkakati bora kukabiliana nao PSG wasiweze kuwadhuru ambapo Ubora wa PSG ni wachezaji wao kucheza na nafasi katikati na nyuma ya mistari ya uzuiaji ya wapinzani wao

Kwa kutambua hilo, Arsenal hawakuingia kwenye mtego wa kwanza wa PSG ambao ni kujenga mashambulizi kuanzia nyuma golini kwao wakiwa na lengo la kuwashawishi Arsenal kwenda kushinikiza wakosee, ili wakivutika na kuwafuata PSG Waweze kupata njia za kupita kama;



- Katikati kwa Vitinha, Ruiz na Neves
- Pembeni kwa Mendez na Hakimi
- Nyuma ya kuta za Arsenal kwa Dembele, Khvicha na Doue

Arsenal wakawa wanazuia kwakufunga njia bila kuweka presha kubwa kwenye mpira huku wakiwa pamoja nyakati nyingi ili kuepuka kuacha nafasi kubwa katikati na nyuma ya mistari yao ya uzuiaji.

3. PSG ilikabiliana vipi na mashambulizi ya kujibu ya Arsenal?

Kwasababu Arsenal ilichagua kucheza nyuma ya mpira nyakati nyingi (Mid & Low Block), ni wazi kuwa ilitegemea mashambulizi ya kujibu (Positives Transitions) kama njia ya kuweza kuifikia na kuidhuru PSG.

PSG walijiandaa na hali hiyo ambapo kila wakiwa na mpira wakihakikisha wanaacha umbo zuri lenye idadi sahihi ya wachezaji kwenye mistari miwili ya nyuma ili kumeza mashambulizi ya kujibu ya Arsenal (Rest Defence/ Offensive Balance).

 


Mfano, nyakati nyingi walikuwa na watu wanne kwenye umbo la 3+2 au 2+3, ambapo;

- Wakishanbulia na umbo la 3-2-5, Vitinha na Ruiz huwa nyuma ya Mendez, Pacho na Marquinhos.

- Wakishambulia na umbo la 2-3-5, Mendez, Vitinha na Ruiz  huwa mbele ya Pacho na Marquinhos.

Umbo hili lilisaidia kumeza mashambulizi ya kujibu ya Arsenal ambayo nyakati nyingi yalikuwa na watu wawili  au wakizidi watatu, Saka, Trossard na Kai, hivyo PSG kuwa na faida kubwa ya Idadi ya watu kuliko Arsenal.

4. PSG Ilikabiliana vipi na Kona za Arsenal?
 


Moja kati ya silaha kubwa ya Arsenal kwa misimu ya karibu ni mipira ya kutenga (Set Pieces) ambapo kati magoli 71 iliyofunga msimu huu kwenye Ligi kuu Uingereza, magoli 29 yametokana na mipira ya aina hiyo kama Kona, Free kick, mirusho na penalti huku magoli ya kona pekee yakiwa 18.

 

Kwa kuzingatia hilo, PSG waliandaa mkakati wa kuzuia kona za Arsenal kwa kuzuia  kwa idadi kubwa ya wachezaji eneo ambalo wanakadiria mara nyingi mpigaji (Saka Mara nyingi) huupeleka mpira kwenye boxi lao (Zonal Marking).


Baada ya hapo huwa rahisi kwa wachezaji wao kushinda mipira ya juu (Aerial Duels) na inayodondoka (Second Balls).

5. Makosa yalizaaje magoli?

Mpira wa miguu ni mchezo wa makosa, licha ya kuwa makocha kupeana wakati mgumu kimbinu, bado makosa ya kiufundi ya wachezaji yalifanya mchezo huo utupe magoli.

 

 -  Arsenal walikuwa wa kwanza kutuonyesha kosa la PSG ambapo waliwakaribisha PSG kwao, kama ilivyo kawaida PSG wanazuia kwa shinikizo kubwa kuanzia kwenye nusu ya mpinzani wao, wakaenda hapo ndipo Arsenal wakapata nafasi ya kupita katikati ya mistari ya uzuiaji ya PSG na kuvuka presha lakini kwasababu ya shinikizo kubwa la PSG bado waliweza kuupora mpira ambapo Hakimi aliufikia lakini wakati wa kuusafisha Kai Havertz akaweka presha tena na kuupora, kujibu shambulizi kwenye nafasi ya wazi hadi kufunga.

 

 - PSG kipindi cha pili kwasababu walipiga kambi sana kwenye theluthi ya mwisho ya Arsenal walifaidika na makosa ya kiufundi ya uzuiaji ya mlinzi wa Arsenal Mosquera ambayo katika harakati za kuwania kupora mpira kutoka kwa Khvicha akajikuta anachelewa sekunde hali iliyomfanya kushindwa kupora mpira na kumchezea faulo winga huyo hatari raia wa Georgia kisha ikazaa mkwaju wa penalti ulipigwa na Dembele.

pmbet
pmbet

Leagues standings

Tanzania Premier League
pmbet
pmbet