Matokeo ya darasa la 7 ya Lionel Messi yavuja, michezo alipiga 10/10
Eric Buyanza
November 26, 2026
Share :

Ripoti ya zamani ya matokeo ya mtihani wa darasa la saba ya nguli wa soka duniani, Lionel Messi, katika Shule ya Msingi ya General Las Heras mjini Rosario, Argentina, imevuja kwenye mitandao ya kijamii.
Kwa mujibu wa taarifa zilizosambazwa na mchambuzi na mwandishi wa habari za michezo, Enock Kobina Essel, nakala hiyo ya ripoti inaonyesha kuwa ingawa Messi alikuwa na ufaulu wa wastani katika masomo ya kawaida darasani, kipaji chake cha soka kilishaanza kujidhihirisha mapema kupitia somo la michezo.
Matokeo yake yalikuwa kama ifuatavyo:
• Elimu ya Michezo (Physical Education): 10/10
• Sanaa na Muziki (Arts and Music): 8/10
• Elimu ya Maadili (Moral Education): 7/10
• Hisabati, Lugha, Maarifa ya Jamii, Lugha ya Kigeni na Teknolojia: 6/10 katika kila somo.
Walimu waliowahi kumfundisha wanakumbuka kuwa Messi alikuwa mwanafunzi mpole, mkimya na mwenye haya akiwa darasani, lakini alibadilika kabisa na kuwa mchangamfu pindi tu alipokanyaga uwanjani na kuwa na mpira miguuni mwake.
Messi mwenyewe aliwahi kukiri katika mahojiano ya nyuma kuwa hakuwa mwanafunzi aliyependa sana kusoma, na kwamba walimu pamoja na wazazi wake walikuwa wakitumia soka kama "silaha" ya kumfanya asome—wakimtishia kumzuia kucheza mpira endapo angefeli mitihani yake.





